Sababu za Kuanzishwa kwa Hizb ut Tahrir

Hizb ut Tahrir ilianzishwa kwa kuitikia kauli ya Mwenyezi Mungu (swt),

[وَلْتَكُن مِّنكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى ٱلْخَيْرِ وَيَأْمُرُونَ بِٱلْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ ٱلْمُنكَرِ ۚوَأُو۟لَٰٓئِكَ هُمُ ٱلْمُفْلِحُونَ‎]

“Na uwe kutokana na nyinyi umma unaolingania kheri na unaoamrisha mema na unaokataza maovu, na hao ndio waliofaulu” [TMQ 3:104]

Kusudio lake lilikuwa kuufufua Ummah wa Kiislamu kutoka katika mporomoko mkubwa ulioufikia, na kuukomboa kutoka katika fikra, mifumo na sheria za Kikafiri, pamoja na utawala na ushawishi wa dola za Kikafiri. Pia inalenga kurejesha Dola ya Kiislamu ya Khilafah ili hukumu kwa kile alichokiteremsha Mwenyezi Mungu (swt) irejee.

Wajibu wa Kisheria wa Kuanzisha Vyama vya Kisiasa

(a) Kuanzishwa kwa Chama kwa kuitikia kauli ya Mwenyezi Mungu (swt), “Na uwe kutokana na nyinyi umma …” ni kwa sababu Mwenyezi Mungu (swt) amewaamuru Waislamu katika aya hii kwamba lazima kuwe na kundi lililopangika kati yao ambalo litafanya kazi mbili: Kwanza, kulingania kheri, yaani kulingania Uislamu; na pili, kuamrisha mema na kukataza maovu.

Amri hii ya kuanzisha kundi lililopangika ni takwa. Hata hivyo, kuna kiunganishi cha kuashiria kwamba hili ni takwa la kukata (amri), kwa sababu kazi ya kundi lililopangika, kama ilivyofafanuliwa katika aya iliyo hapo juu (kulingania Uislamu, kuamrisha mema na kukataza maovu), ni wajibu juu ya Waislamu; wanapaswa kuitekeleza kama ilivyothibitishwa katika aya nyingi za Qur’an na hadithi za Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) zinazoashiria hilo.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema,

‏ «وَالَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَتَأْمُرُنَّ بِالْمَعْرُوفِ وَلَتَنْهَوُنَّ عَنِ الْمُنْكَرِ أَوْ لَيُوشِكَنَّ اللَّهُ أَنْ يَبْعَثَ عَلَيْكُمْ عِقَابًا مِنْهُ ثُمَّ تَدْعُونَهُ فَلاَ يُسْتَجَابُ لَكُمْ» ‏

“Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mkononi Mwake, lazima muamrishe mema na mkataze maovu, la sivyo Mwenyezi Mungu atakuwa karibu kuwaletea adhabu kutoka Kwake. Na kisha mkiomba Kwake (kumuomba), Hatawajibu.”

Hadithi hii ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ni kiunganishi kinachoonyesha kwamba takwa (katika aya iliyo hapo juu) ni la kukata, na amri ni wajibu.

(b) Ukweli kwamba kundi hili lililopangika ni chama cha kisiasa unaeleweka kwa aya inapowataka Waislamu kuunda kutoka kwao wenyewe kundi, na kwamba kazi ya kundi hili imefafanuliwa kuwa kulingania Uislamu, kuamrisha mema, na kukataza maovu.

Kutekeleza jukumu la kuamrisha mema na kukataza maovu ni pamoja na kuwaamrisha watawala kufanya mema na kuwakataza kutokana na maovu. Kipengele hiki, ambacho kinamaanisha kuwahisabu watawala na kuwapa nasaha ni muhimu zaidi, na kazi hii ni ya kisiasa; ni mojawapo ya vitendo muhimu zaidi vya kisiasa na mojawapo ya kazi kuu za vyama vya kisiasa. Aya hiyo basi inaashiria wajibu wa kuanzisha vyama vya kisiasa. Hata hivyo, aya hiyo inaweka sharti kwamba vyama hivi vya kisiasa vinapaswa kuwa vya Kiislamu, kwa sababu kazi ya vyama hivi, kama ilivyofafanuliwa na aya ni kulingania Uislamu, kuamrisha mema na kukataza maovu, kulingana na sheria za Uislamu, ambayo haiwezi kufanywa isipokuwa na makundi na vyama ambavyo ni vya Kiislamu.

Chama cha Kiislamu ni kile kilichoanzishwa juu ya aqeedah ya Kiislamu, kinachochukua fikra, sheria na ufumbuzi wa Kiislamu, na kufuata njia ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw). Kwa hivyo, hairuhusiwi kwa Waislamu kuunda makundi kwa msingi mwingine usio kuwa Uislamu kama fikra na njia, kwa sababu Mwenyezi Mungu (swt) amewaamuru wasifanye hivi, na kwa sababu Uislamu ndio itikadi sahihi pekee ulimwenguni. Ni itikadi ya ulimwengu wote inayokubaliana na maumbile ya mwanadamu, na inashughulika na wanadamu kama wanadamu. Hivyo Uislamu unashughulika na maumbile ya mwanadamu na mahitaji ya kimaumbile, na kuyapanga na kutoshelezwa kwake kwa usahihi, bila kuyakandamiza au kuyapa uhuru wa kupitiliza, au kuruhusu umbile moja kushinda jingine. Kwa jumla, ni itikadi kamili inayopanga mambo ya maisha.

© Mwenyezi Mungu (swt) amefanya kuwa ni lazima kwa Waislamu kujifunga na Uislamu na sheria zake pekee, iwe ni katika kupanga uhusiano wao na Muumba wao, kama vile sheria za imani na ibada za kiibada, au na nafsi zao, kama vile sheria za maadili, chakula na mavazi au na wengine kama vile sheria za muamalat na utungaji sheria.

Mwenyezi Mungu (swt) pia amewawajibisha Waislamu kutekeleza Uislamu katika mambo yote ya maisha, kutawala kwa Uislamu na kufanya katiba yao na sheria zao mbalimbali kwa msingi wa sheria za Shari’ah ambazo zimetolewa kutoka katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu (swt) na Sunnah za Mtume Wake (saw). Mwenyezi Mungu (swt) anasema,

[فَٱحْكُم بَيْنَهُم بِمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ ۖوَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَآءَهُمْ عَمَّا جَآءَكَ مِنَ ٱلْحَق]

“Basi hukumu baina yao kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao ukaacha Haki iliyokujia.” [TMQ 5:48]

[وَأَنِ ٱحْكُم بَيْنَهُم بِمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَآءَهُمْ وَٱحْذَرْهُمْ أَن يَفْتِنُوكَ عَنۢ بَعْضِ مَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ إِلَيْكَ ۖ]

“Na hukumu baina yao kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao, na tahadhari nao wasije wakakufitini ukaacha baadhi ya yale aliyokuteremshia Mwenyezi Mungu.” [TMQ 5:49]

Mwenyezi Mungu (swt) alizingatia kutotawala kwa Uislamu kama kitendo cha Kufru. Mwenyezi Mungu (swt) anasema,

[وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ فَأُو۟لَٰٓئِكَ هُمُ ٱلْكَٰفِرُونَ]

“Na wasiohukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri.” [TMQ 5:44]

Itikadi nyingine isipokuwa Uislamu, kama Ubepari na Ukomunisti (ambao unajumuisha Ujamaa), ni itikadi potofu zinazopingana na maumbile ya mwanadamu na zimetungwa na wanadamu. Upotofu wao umedhihirika, kasoro zao zimeonekana, na zinapingana na Uislamu na sheria zake, hivyo kuzichukua ni haramu. Kuzikumbatia na kuzilingania ni haramu na kuanzisha makundi kwa msingi wake pia ni haramu. Kwa hivyo, Waislamu wanapoanzisha makundi lazima yawe kwa msingi wa Uislamu pekee kama fikra na njia, na ni haramu kwa Waislamu kuanzisha makundi kwa msingi wa Ubepari, Ukomunisti, Ujamaa, Uzalendo, Utaifa, Ukabila au Umasoni. Hivyo, ni haramu kwa Waislamu kuanzisha vyama vya Kikomunisti, Kisoshalisti, Kibepari, Kizalendo, Kitaifa, Kikabila au Kimasoni au kujihusisha na vyama hivyo au kuvipigia debe, kwani ni vyama vya Kikafiri vinavyolingania Kufru. Mwenyezi Mungu (swt) anasema,

[وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ ٱلْإِسْلَٰمِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِى ٱلْـَٔاخِرَةِ مِنَ ٱلْخَٰسِرِينَ]

“Na anayetafuta dini isiyo kuwa Uislamu, haitakubaliwa kwake, na yeye Akhera atakuwa katika wenye kupata hasara.” [TMQ 3:85]

Na aya iliyo hapo juu inasema, “inayolingania kheri” [TMQ 3:104] yaani Uislamu.

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema,

»مَنْ أَحْدَثَ فِي أَمْرِنَا هَذَا مَا لَيْسَ مِنْهُ فَهُوَ رَدٌّ‏«

“Yeyote atakayefanya kitendo ambacho si kulingana na amri yetu (yaani Uislamu), kimekataliwa.”

Na yeye (saw) amesema,

»لَيْسَ مِنَّا مَنْ دَعَا إِلَى عَصَبِيَّةٍ«

“Yeyote anayelingania 'asabiyyah (ukabila) si mmoja wetu.”

(d) Ufufuo wa Ummah wa Kiislamu kutoka katika mporomoko ambao umefikia, na ukombozi wake kutoka katika fikra, mifumo na sheria za Kikafiri, na kutoka katika utawala na ushawishi wa dola za Kikafiri - yote haya lazima yafikiwe kwa kuunyanyua kiakili kupitia mabadiliko ya kimsingi na ya kina ya fikra na dhana zilizopelekea mporomoko wake na kwa kuleta ndani yake fikra na dhana za Kiislamu, na kwa kuunda mtazamo wake kuelekea maisha kulingana na fikra na sheria za Uislamu pekee.

Jambo lililopelekea mporomoko huu wa kushtua, ambao hauufai, ni udhaifu mkubwa uliotokea katika akili za Waislamu katika uelewa wao na utendaji wao wa Uislamu. Hii ilitokana na mambo kadhaa yaliyofunika fikra na njia ya Uislamu kuanzia wakati wa karne ya 2 baada ya hijrah hadi sasa. Mambo haya ya kufunika yalitokana na vitu vingi, maarufu zaidi vikiwa:

  1. Kuingia kwa falsafa za Kihindu, Kiajemi na Kigiriki, na juhudi za baadhi ya wanafalsafa wa Kiislamu kupatanisha falsafa hizi na Uislamu licha ya mgongano kamili kati yao.
  2. Hila za watu wenye chuki dhidi ya Uislamu waliopromoti fikra na sheria fulani ambazo si za Uislamu, ili kuuchafua na kuwapotosha Waislamu mbali nao.
  3. Uzembe katika kutumia lugha ya Kiarabu katika kuelewa na kufikisha Uislamu, na kujitenga kwake na Uislamu katika karne ya 7 AH, licha ya ukweli kwamba Uislamu hauwezi kueleweka bila lugha ya Kiarabu. Zaidi ya hayo, utoaji wa sheria mpya kwa hali na masuala mapya kupitia ijtihad hauwezi kupatikana bila lugha ya Kiarabu.
  4. Uvamizi wa kimishonari, kiutamaduni na kisha kisiasa kuanzia wakati wa karne ya 17 CE ulioanzishwa na dola za Kikafiri za Magharibi zilizotaka kupotosha uelewa wa Waislamu wa Uislamu na kuwaweka mbali nao, kwa madhumuni ya kuubomoa.

(e) Majaribio na harakati kadhaa, za Kiislamu na zisizo za Kiislamu, ziliibuka ili kuwafufua Waislamu, lakini zote zilishindwa. Hazikuweza kuwafufua Waislamu wala kuzuia mporomoko wao mkubwa. Sababu ya kushindwa kwa majaribio haya na makundi yaliyoanzishwa ili kuwafufua Waislamu kwa Uislamu ilitokana na sababu mbalimbali; hizi zilikua kama ifuatavyo:

  1. Kukosekana kwa uelewa sahihi wa fikra ya Kiislamu kwa wale watu waliochukua jukumu la kuwafufua Waislamu. Hii ni kwa sababu waliathiriwa na mambo fulani ya kufunika. Walikuwa wakilingania Uislamu kwa namna ya jumla isiyofafanuliwa, bila kufafanua fikra na sheria ambazo walitaka kuwafufua Waislamu kwazo, kutatua matatizo yao, na kuzitekeleza. Hii ilitokana na ukosefu wa uwazi wa fikra na sheria hizi katika akili zao. Walifanya hali halisi kuwa chanzo cha kufikiri kwao, ambapo fikra zao zilitolewa, na walijaribu kutafsiri Uislamu na kuuelezea kwa kutumia maana ambazo maandiko yake yanakataza. Walifanya hivyo ili kukubaliana na hali iliyopo ingawa ilipingana na Uislamu. Hawakufanya hali halisi kuwa somo la fikra zao ili kuibadilisha kulingana na Uislamu na sheria zake. Badala yake, walilingania uhuru na demokrasia, na mifumo ya Kibepari na Kisoshalisti na kuielewa kuwa inatokana na Uislamu, ingawa inapingana nao kabisa.

  2. Kukosekana kwa njia sahihi na iliyofafanuliwa wazi ambayo kwayo fikra na sheria za Kiislamu zinatekelezwa. Makundi na watu binafsi walifikisha wazo la Kiislamu kwa njia ya kubuni na kwa namna iliyogubikwa na utata. Walitazamia ufufuo wa Uislamu kupitia ujenzi wa misikiti na uchapishaji wa vitabu, au kwa uanzishwaji wa mashirika ya ustawi na ushirika, au kwa elimu ya maadili na marekebisho ya watu binafsi; huku wakipuuza ufisadi wa jamii na utawala wa fikra, sheria na mifumo ya Kikafiri juu yake. Walidhani kwamba marekebisho ya jamii yanapatikana kwa kurekebisha watu wake binafsi, licha ya ukweli kwamba marekebisho yake yanapatikana tu kwa kurekebisha fikra, hisia na mifumo yake, ambayo ingepelekea marekebisho ya wanachama binafsi wa jamii, kwa sababu jamii haiundwi na seti ya watu binafsi pekee, bali inaundwa na watu binafsi na mahusiano, yaani watu binafsi, fikra, hisia na mifumo. Hii ilikuwa ndiyo njia hasa ambayo Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alifanya kazi kubadilisha jamii ya kijahili kuwa jamii ya Kiislamu. Alianza kazi ya kubadilisha itikadi zilizopo kuwa fikra za aqeedah ya Kiislamu, na kubadilisha fikra, dhana na mila za kijahili kuwa fikra, dhana na sheria za Kiislamu, na hivyo kubadilisha hisia za watu kutoka kushikamana na itikadi, fikra na mila za kijahili hadi kushikamana na aqeedah ya Kiislamu na fikra za Uislamu na sheria zake. Hii ilitokea mpaka Mwenyezi Mungu (swt) alipomrahisishia mabadiliko ya jamii huko Madinah kiasi kwamba umati mkubwa wa watu huko Madinah walikuja kuikubali itikadi ya Uislamu na kuchukua fikra, dhana na sheria zake. Kisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na Masahaba zake walihamia Madinah baada ya kuhitimisha kiapo cha pili cha 'Aqabah, ambapo alianza kutekeleza sheria za Uislamu na kwa hili alisimamisha jamii ya Kiislamu.

    Harakati nyingine zilibeba fikra ya Kiislamu kwa njia za kimaada na kuunga mkono kuchukua silaha. Hata hivyo, walishindwa kutofautisha kati ya Dar al-Islam na Dar al-Kufr. Pia hawakuelewa tofauti kati ya namna ya kufikisha da’wah kinyume na kubadilisha uovu ndani ya hali hizi mbili tofauti. Leo tunaishi ndani ya Dar al-Kufr kwa sababu kila mahali karibu nasi sheria za Kufru zinatumika, na katika hali hii jamii inafanana na Makkah wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alipotumwa na Mwenyezi Mungu (swt). Kwa hivyo, kufikisha wito wa Uislamu katika hali hii lazima kufanywe kupitia da’wah na hatua za kisiasa na si kwa njia za kimaada. Hii ni kwa mujibu wa jinsi Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alivyofikisha da’wah huko Makkah, ambapo alizuia kazi yake kwenye da’wah ya Uislamu na hakukimbilia njia za kimaada. Lengo katika hali ya sasa si kubadilisha mtawala anayetawala kwa Kufru katika Dar al-Islam; lengo ni badala yake kubadilisha Dar al-Kufr yote, ikiwa ni pamoja na fikra na mifumo yake. Mabadiliko yake yanapatikana kwa kubadilisha fikra, hisia na mifumo iliyoenea ndani yake, kama Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alivyofanya huko Makkah.

    Ikiwa katika Dar al-Islam, ambayo inatawaliwa kulingana na ufunuo wa Mwenyezi Mungu (swt), mtawala wake atatawala kwa Kufru ya wazi basi Waislamu lazima wakataze hilo, ili arejee kwenye kutawala kulingana na Uislamu. Ikiwa hatatubu, inakuwa ni lazima juu ya Waislamu kuchukua silaha dhidi yake ili kumlazimisha kurejea kwenye kutawala kwa ufunuo wa Mwenyezi Mungu (swt). Hii ndiyo njia sahihi iliyoelezewa katika hadithi iliyosimuliwa na 'Ubada ibn as-Samit, “…na kwamba msigombanie haki ya watawala ya kutawala mpaka mkaone ukafiri wa wazi (waziwazi) ambao mna ushahidi juu yake kutoka kwa Mwenyezi Mungu.” Na imeelezewa katika hadithi iliyosimuliwa na 'Auf ibn Malik katika kitabu cha Imam Muslim kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) aliulizwa na Masahaba zake, “Je, tusiwakabili (watawala) kwa upanga?” Mtume wa Mwenyezi Mungu alijibu, “Hapana, mradi tu wanasimamisha salah miongoni mwenu.” Kusimamisha salah katika hadithi hii kwa hakika ni ishara ya kutawala kwa Uislamu. Hadithi hizi mbili zinahusu kumhisabu mtawala Mwislamu katika Dar al-Islam, zikionyesha namna ya kuhojiwa kwake na mazingira yanayozunguka matumizi ya nguvu za kimaada kupinga kuibuka kwa Kufru ya wazi (waziwazi) katika Dar al-Islam wakati hapo awali haikuwepo.

(f) Kuhusu hitajio la kufanya kazi kurejesha Dola ya Khilafah, na hivyo kutawala kwa kile alichokiteremsha Mwenyezi Mungu (swt), hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu (swt) amewawajibisha Waislamu kujifunga na sheria zote za Shari’ah, na Yeye (swt) amefanya kuwa ni wajibu juu yao kutawala kwa ufunuo Wake (swt). Hili lisingewezekana isipokuwa kuwepo Dola ya Kiislamu na Khalifa anayetekeleza Uislamu juu ya watu.

Tangu Khilafah ilipobomolewa baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, Waislamu wamekuwa wakiishi bila Dola ya Kiislamu na bila utawala wa Kiislamu. Kwa hivyo, kazi ya kurejesha Khilafah, pamoja na kutawala kwa kile alichokiteremsha Mwenyezi Mungu (swt) ni wajibu wa kukata ambao Uislamu unauweka juu ya Waislamu wote. Ni wajibu usioepukika (usio na chaguo, au kuridhika). Uzembe wowote katika kutekeleza jukumu hili ni dhambi kubwa, ambayo kwa kuifanya Mwenyezi Mungu (swt) anaadhibu vikali. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema,

«وَمَنْ مَاتَ وَلَيْسَ فِي عُنُقِهِ بَيْعَةٌ، مَاتَ مِيتَةً جَاهِلِيَّةً»

“Yeyote anayekufa bila kuwa na bay’ah (kiapo cha utii kwa Khalifa) shingoni mwake, anakufa kifo cha kijahili.”

Na kushindwa kuzingatia jukumu hili ni kupuuza mojawapo ya amri muhimu zaidi za Uislamu, kwani utekelezaji wa Uislamu unategemea amri hii. Hata kusimamisha Uislamu katika mwenendo wa maisha kunategemea hilo, na, ‘Chochote kinachohitajika ili kutimiza wajibu ni wajibu chenyewe.’

Kwa hivyo Hizb ut-Tahrir ilianzishwa na uundaji wake ulitegemea aqeedah ya Kiislamu. Ilichukua dhana na sheria hizo za Uislamu ambazo zinahitajika kutekeleza lengo lake. Imepunguza mapungufu na sababu zilizopelekea kushindwa kwa harakati zilizoanzishwa kuwafufua Waislamu kwa Uislamu. Chama kilielewa kiakili na kwa kina wazo na njia kutoka katika Qur’an, Sunnah, Ijma’ ya Masahaba na Qiyas (kipimo). Ilichukua hali halisi kama somo la fikra yake ili kuibadilisha kulingana na sheria za Uislamu. Ilijitolea kwa njia ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) katika kazi yake ya kufikisha da’wah huko Makkah mpaka aliposimamisha Dola huko Madinah. Chama kilifanya aqeedah, fikra na sheria zake kuwa ushirika unaowafunga pamoja wanachama wake.

Kwa hivyo inastahili kwamba Ummah uikumbatie na kuendelea nayo; kwa kweli Ummah lazima uikumbatie na kuendelea nayo kwa sababu ni chama pekee kinachochakata wazo lake, kinachotabiri njia yake, kinachoelewa suala lake, na kujitolea kufuata seerah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) bila kupotoka kwayo, na bila kuruhusu chochote kuishawishi isifikie lengo lake.